EU yalaani kuhukumiwa kifo wananchama wa Ikhwani, Misri
(last modified Wed, 12 Sep 2018 01:20:26 GMT )
Sep 12, 2018 01:20 UTC
  • EU yalaani kuhukumiwa kifo wananchama wa Ikhwani, Misri

Umoja wa Ulaya umelaani hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama moja nchini Misri, dhidi ya makumi ya wanachama wa harakati ya Ikhwanul Muslimin.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, msemaji wa masuala ya kidiplomasia wa EU ameeleza wasiwasi mkubwa ulionao umoja huo, kuhusu mchakato wa kesi dhidi ya wanaharakati hao.

Amesema EU inahisi kuwa kesi za washukiwa hao hazikuendeshwa kiuadilifu na kwamba umoja huo haukubaliana na hukumu hizo katika hali yoyote ile.

Siku ya Jumapili, Michelle Bachelet Mkuu mpya wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ameitolea mwito mahakama ya rufaa ya Misri kutengua hukumu za vifo zilizotolewa na mahakama moja nchini humo dhidi ya viongozi na wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin.

Huku akikosoa sheria inayotoa kinga kwa maafisa usalama wa ngazi za juu waliofanya uhalifu dhidi ya raia, Bachelet amesisitiza kuwa, iwapo hukumu hizo za kunyongwa wafuasi wa Ikhwani zitatekelezwa, hatua hiyo itakuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu. 

Mahakama Misri

Mahakama moja nchini Misri siku ya Jumamosi iliwahukumu watu 75 adhabu ya kifo wakiwemo viongozi watajika wa harakati ya Ikhwanul Muslimin kwa kosa la kushiriki katika maandamano ya amani na mgomo wa kuketi chini mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani Rais Mohamed Morsi wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Katika maandamano hayo, maafisa usalama wa Misri waliwaua mamia ya waandamanaji. 

Tags