Sheria ya kura ya maoni kuhusu katiba ya Libya yapasishwa
Bunge la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi limefanya kikao cha dharura na kupasisha suala la kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi hiyo.
Abdullah Bliheeq msemaji wa Bunge la Libya lenye makao yake katika mji wa Tobruk amesema kuwa licha ya kupasishwa sheria hiyo Bunge hilo pia limechukua uamuzi wa kufanya kikao cha kuchunguza marekebisho, lengo likiwa ni kuzuia kubadilishwa sheria hiyo.
Spika wa bunge hilo la Libya, Aguila Saleh amewataka wabunge kuitisha kikao kujadili sheria hiyo ya kura ya maoni.
Libya imetumbukia katika hali ya machafuko, hujuma za makundi yenye silaha na kuwa ngome ya makundi ya kigaidi kutokana na matukio yaliyojiri nchini humo mwaka 2011 na uingiliaji wa Marekani na muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi (Nato) nchini humo.
Ushindani wa kisiasa umeifanya Libya kuwa na serikali mbili, moji ikiwa mashariki mwa nchi, na serikali ya umoja wa kitaifa yene makao yake katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli. Bunge la Tobruk linaungwa mkono na Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar huku serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayez al Sarraj ikiungwa mkono na nchi za Magharibi hususan Marekani.