Utekaji nyara wa kutumia silaha waongezeka Kinshasa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48211-utekaji_nyara_wa_kutumia_silaha_waongezeka_kinshasa_drc
Familia za wahanga wa vitendo vya utekaji nyara wa kutumia silaha katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa wameelekeza kidole cha lawama kwa mashirika ya usalama ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 17, 2018 23:27 UTC
  • Utekaji nyara wa kutumia silaha waongezeka Kinshasa DRC

Familia za wahanga wa vitendo vya utekaji nyara wa kutumia silaha katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa wameelekeza kidole cha lawama kwa mashirika ya usalama ya nchi hiyo.

Malalamiko hayo yameongezeka baada viwiliwili kadhaa vya watu waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha na baadaye kuuawa kuokotwa katika eneo la Kalamu mjini Kinshasa.

Vyombo vya habari vimelinukuu jeshi la polisi la Kinshasa likisema kuwa limeokota viwiliwili vinne vya watu walioripotiwa kupotea lakini duru za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa viwiliwili hivyo ni vya watu sita na wote ni vijana ambao siku ya Ijumaa walitekwa nyara na watu waliokuwa wameziba nyuso zao. Viwiliwili vyote hivyo viliokotwa juzi Jumapili katika eneo la Kalamu lenye harakati nyingi za watu mjini Kinshasa.

Eneo lenye harakati nyingi la Kalamu mjini Kinshasa, DRC

 

Vyombo hivyo vya habari vinasema kuwa, baadhi ya familia za wahanga hao zinadai kuwa maafisa usalama wa serikali ndio waliofanya jinai hiyo. Hata hivyo Jenerali Sylvano Kasongo Kitenge, mkuu wa jeshi la polisi mjini Kinshasa amekanusha vikali madai hayo na kuahidi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji hayo.

Udhaifu wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika kupambana na makundi ya waasi na wanamgambo wenye silaha ndio unaodaiwa kuwa sababu kuu ya ukosefu wa amani na utulivu katika nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.