Sep 21, 2018 13:46 UTC
  • Hujuma za kigaidi zalipuka tena Msumbiji, 12 wauawa

Kundi la kigaidi linaloaminika kuwa na mfungamano na al-Shabaab ya Somalia limevamia kijiji kimoja katika mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji na kuua watu 12 na kujeruhiwa wengine kadhaa.

Afisa wa Afya katika mkoa wa Cabo Delgado ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, magaidi hao walishambulia kijiji cha Paqueue usiku wa kuamkia leo, na kuua watu 10 kwa kuwafyatulia risasi huku wengine wawili wakiteketea kwa moto hadi kufa baada ya wavamizi hao kuchoma moto nyumba 55 katika kijiji hicho.

Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe akihofia usalama wake amesema watu wengine 14 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya kigaidi ya jana usiku.

Katika hatua nyingine, afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Msumbiji ameuawa baada ya msafara wa magari ya jeshi kushambuliwa na genge la wabeba silaha waliokuwa wamevalia magwanda ya kijeshi katika kijiji cha Paqueue karibu na mpaka wa nchi hiyo na Tanzania.

Maafisa usalama nchini Msumbiji

Kwa mujibu shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, watu wasiopungua 50 wameuawa katika mashambulizi yanayoaminika kuwa ya kigaidi huko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Mei mwaka huu hadi sasa.

Kundi hilo la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda lilikiri kuhusika na mashambulizi ya mwezi Oktoba mwaka jana, dhidi ya kituo cha polisi na kambi ya jeshi katika mji wa Mocimboa da Praia nchini Msumbiji, ambapo watu 16 waliuawa wakiwemo maafisa wawili wa jeshi la polisi.

Tags