Afrika Kusini yakanusha taarifa za kurejea tena balozi wake mjini Tel Aviv
(last modified Thu, 27 Sep 2018 03:00:13 GMT )
Sep 27, 2018 03:00 UTC
  • Afrika Kusini yakanusha taarifa za kurejea tena balozi wake mjini Tel Aviv

Serikali ya Afrika Kusini imekanusha taarifa zilizoenea kwamba, imemrejesha huko Tel Aviv balozi wake ambaye ilimwita nyumbani mwezi Mei mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Uhusiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini imeeleza kuwa, Sisa Ngombane aliyekuwa balozi wake huko Tel Aviv amesafiri kuelekea katika mji huo kwa mambo yake binafsi na kwa ajili ya kushughulikia masuala yake ya kifamilia.

Taarifa hiyo imesisitiza kwamba, Afrika Kusini haijamtuma Sisa Ngombane kurejea Tel Aviv kama balozi wake, bali mwanadiplomasia huyu yupo huko Israel kwa ajili ya masuala yake binafsi na kwamba, mara tu atakapomaliza kazi yake atarejea nchini Afrika Kusini.

Sisa Ngombane, balozi wa Afrika Kusini mjini Tel Aviv (wa katikati)

Gazeti la Israel la Times liliandika hivi karibuni katika moja ya matoleo yake kwamba, Sisa Ngombane amerejea kwa siri mjini Tel Aviv na ameanza tena shughuli zake kama balozi wa Afrika Kusini katika mji huo.

Aidha Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala dhalimu wa Israel ikatangaza kuthibitisha taarifa za kuurejea mjini Tel Aviv balozi wa Afrika Kusini.

Hata hivyo serikali ya Afrika Kusini imesisitiza kuwa, taarifa hizo hazina ukweli na kwamba, serikali ya Pretoria haijamtaka Sisa Ngombane arejee Tel Avuiv na kuendelea na majukumu yake kama balozi.

Serikali ya Afrika Kusini ilimwita nyumbani balozi wake, mwezi Mei mwaka huu ikilalamikia vitendo vya ukatili vya wanajeshi wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.