Wanajeshi 8 wauawa katika mripuko kaskazini mwa Burkina Faso
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48410
Askari wanane wa jeshi la Burkina Faso wamepoteza maisha kufuatia mripuko wa bomu uliotokea jana Jumatano kaskazini mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 27, 2018 03:00 UTC
  • Wanajeshi 8 wauawa katika mripuko kaskazini mwa Burkina Faso

Askari wanane wa jeshi la Burkina Faso wamepoteza maisha kufuatia mripuko wa bomu uliotokea jana Jumatano kaskazini mwa nchi.

Rais Roch Marc Christian Kabore wa nchi hiyo amethibitisha habari ya kutokea mripuko huo na kusema kuwa, msafara wa magari ya jeshi uliokuwa ukitokea mji wa Baraboule mkoani Soum, kuelekea mjini Djibo, ulikanyaga bomu la kutegwa ardhini ambalo anasisitiza kuwa lilitegwa na 'maadui wa taifa'.

Amesema, "Mashambulizi ya kikatili na kiuoga ya aina hii katu hayatizima ari ya kulinda mipaka yetu na kuhuisha amani na usalama kwa ajili ya furaha na ufanisi wa watu wa Burkina Faso."

Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, maafisa usalama wapatao saba wa nchi hiyo waliuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu jingine la kutegwa ardhini, mashariki mwa nchi.

Rais Roch Marc Christian Kabore wa Burkinabe

Kadhalika mwezi Mei mwaka huu, watu wenye silaha walifanya shambulizi katika mji wa Boulekessi ambao uko karibu na mpaka wa Burkina Faso na Mali, na kuua raia 12.

Wavamizi hao walikabiliwa na majibu kutoka kwa wanajeshi wa kikosi cha pamoja cha kundi la nchi za Sahel Afrika walioko kwenye eneo hilo.