Sep 28, 2018 14:33 UTC
  • Kamisheni ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi yaongezewa muda

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeiongezea muda wa mwaka mmoja mwingine kamisheni ya uchunguzi ya umoja huo kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Burundi.

Nchi 47 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo zimelipigia kura azimio la kuongezewa muda wa mwaka mmoja mwingine kamisheni hiyo ya uchunguzi ambapo nchi 23 zimepiga kura ya ndio, 7 zimepiga kura ya hapana na wanachama 17 wamejizuia kupiga kura.

Azimio hilo mbali na kuiongezea muda wa mwaka mmoja kamisheni ya kuchunguza hali ya haki za binadamu nchini Burundi limelaani vitendo vya aina yoyote ile vya utumiaji mabavu vinavyofanywa na upande wowote ule nchini humo.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ambaye serikali yake inatuhumiwa kukiuka haki za binadamu 

Katika ripoti yake iliyoitoa mwezi huu, Kamisheni ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi ilisema kuwa, katika kipindi cha mwaka 2017 na 2018 ukiukaji wa haki za binadamu umeshadidi nchini humo na kwamba, waliohusika zaidi na jinai hizo ni vyombo vya intelejinsia, polisi, jeshi na Jumuiya ya Vijana ya chama tawala cha CNDD-FDD.

Serikali ya Burundi imekuwa ikilituhumu Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba, limekuwa likitia chumvi kwenye ripoti zake kuhusiana na haki za binadamu nchini Burundi na kutanguliza mbele utashi wa kisiasa badala ya ukweli halisi wa mambo.

Burundi ilitumbukia katika machafuko ya kisiasa  mapema mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwa atagombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu; hatua ambayo wapinzani walisema ilikuwa kinyume na katiba ya nchi hiyo. 

Tags