Aliyekuwa kamanda wa al-Shabaab anyimwa idhini ya kuwania urais Somalia
(last modified Sat, 06 Oct 2018 03:50:35 GMT )
Oct 06, 2018 03:50 UTC
  • Aliyekuwa kamanda wa al-Shabaab anyimwa idhini ya kuwania urais Somalia

Serikali ya Mogadishu imemnyima kibali cha kugombea urais wa jimbo moja la Somalia, aliyekuwa Naibu Kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na pia msemaji wa zamani wa genge hilo la ukufurishaji, Mukhtar Robow Abu Mansur, ambaye mwaka jana alijisalimisha kwa jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Taarifa ya Wizara ya Usalama wa Ndani nchini humo imesema kuwa, Robow hawezi kuruhusiwa kugombea kiti cha Ugavana katika jimbo la Kusini Magharibi kwa kuwa angali chini ya vikwazo vya jamii ya kimataifa ikiwemo Polisi ya Kimataifa Interpol.

Robow alitangaza siku ya Alkhamisi akiwa mjini Baidoa kuwa atagombea urais wa jimbo hilo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 17.

Agosti mwaka jana, Robow alijisalimisha kwa jeshi la nchi hiyo katika mji wa Hudur, kusini magharibi mwa nchi. Kamanda huyo mwandamizi wa zamani wa al-Shabaab alichukua umauzi huo miezi miwili baada ya Marekani kumuondoa katika orodha ya magaidi hatari inaowasaka.

Robow (katikati) akiongea kwa niaba ya al-Shabaab enzi zake

Robow alidumu kwenye orodha kwa miaka mitano ambapo US ilikuwa imetangaza zawadi ya Dola milioni 5 kwa yeyote ambaye angemkamata au angetoa taarifa ya kupelekea kukamatwa kwake.

Baadhi ya wadadisi wa mambo nchini Somalia wamekuwa wakisisitiza kuwa, iwapo magaidi walioweka silaha chini na kujisalimisha hawatapandishwa kizimbani kutokana na jinai walizozifanya huko nyuma, basi ni muhali Somalia kurejea katika amani.

Tags