Wafungwa wazusha ghasia Sudan Kusini, waiba silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48629-wafungwa_wazusha_ghasia_sudan_kusini_waiba_silaha
Hali ya taharuki imetanda katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, baada ya mamia ya wafungwa katika gereza moja kuvunja ghala la silaha na kukabiliana na walinzi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 07, 2018 07:43 UTC
  • Wafungwa wazusha ghasia Sudan Kusini, waiba silaha

Hali ya taharuki imetanda katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, baada ya mamia ya wafungwa katika gereza moja kuvunja ghala la silaha na kukabiliana na walinzi.

Duru za kiusalama zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, Gereza la Blue House kwa sasa limezingirwa na maafisa usalama kwa upande wa nje, huku wafungwa hao wakilidhibiti kwa upande wa ndani.

Habari zaidi zinasema kuwa, wafungwa 200 kati ya 400 wa jela hiyo wamefanikiwa kuzusha vurumai hizo na kutwaa silaha kwa msaaada wa baadhi ya askari wa gereza hilo.

Ramani ya Sudan Kusini

Serikali ya Juba imewaachia huru makumi ya wafungwa wa kisiasa tangu Rais Salva Kiir aitishe mazungumzo ya amani yaliyoanza mwezi Mei, mwaka jana 2017, akiwemo Justine Manawila Bilal ambaye alikuwa akituhumiwa kumuunga mkono kiongozi wa upinzani na aliyekuwa Makamu wa Rais, Riek Machar.

Taifa changa la Sudan Kusini limedumu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka minne sasa.