Al-Shabaab ya Somalia yaua 5 kwa tuhuma za ujasusi
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab la Somalia lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limewaua kwa kuwamiminia risasi watu watano kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya vyombo vya kiintelejensia vya Marekani, Uingereza na Somalia.
Genge hilo la kitakfiri kupitia radio yake ya Andalus limethibitisha kutekeleza hukumu hiyo jana Jumanne katika mji wa Jilib eneo la Jubba ya Kati.
Mamia ya wakazi wa mji huo wakiwemo wanawake na watoto wadogo wamelazimishwa kutazama watano hao wakiuawa hadharani kwa kumiminiwa risasi, huku wakiwa wamefungwa kwenye vigingi.
Hii sio mara ya kwanza kwa genge hilo la kitakfiri kutekeleza ukatili wa aina hii kadamnasi ya watu nchini Somalia.
Januari mwaka huu, wanachama wa kundi hilo waliwaua kwa kuwamiminia risasi watu wengine watano kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya Kenya, Somalia na Ethiopia, miezi michache baada ya kuwaua kwa kuwakata vichwa watu wanne walioshukiwa kuwa majasusi, kusini mwa Somalia.
Kabla ya hapo, wazee wanane wa vijiji vya eneo la Galmudug nchini Somalia waliuawa kwa kukatwa vichwa na kundi hilo la kigaidi, eti kwa kuwashawishi wakazi wa maeneo hayo kutolipa kodi na 'zaka' wanazotozwa kwa nguvu na al-Shabaab.