Oct 14, 2018 07:06 UTC
  • Watu 16 wauawa katika shambulizi la kigaidi Somalia

Kwa akali watu 16 wameuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika mji wa Baidoa nchini Somalia.

Kanali Ahmed Muse, afisa wa Jeshi la Somalia amesema watu wengine 30 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya jana Jumamosi, iliyolenga migahawa miwili mjini Baidoa, yapata kilomita 250 magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limetangaza kupitia radio yake ya kipropaganda ya Andalusia kuhusika na hujuma hiyo na kusema kuwa, shambulizi hilo ni sehemu ya wimbi la mashambulizi yanayolenga migawaha inayomilikiwa na waziri wa zamani wa Somalia, Mohamed Aden Fargeti, ambaye anatazamiwa kugombea urais wa moja ya majimbo ya nchi hiyo mwezi Novemba mwaka huu.

Wanachama wa al-Shabaab

Mapema mwezi jana, watu sita waliuawa baada ya gaidi mmoja kushambulia kwa bomu ofisi ya serikali za mitaa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Magaidi wakufurishaji wa al-Shabaab wanaofungamana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wanaendesha kampeni ya mauaji kwa lengo la kuiangusha serikali ya Somalia yenye makao yake Mogadishu na ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Tags