Wahajiri Wakongomani warejea nyumbani kwa wingi baada ya kufukuzwa Angola
Wahajiri Wakongomani na maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesema kuwa makumi ya raia wa nchi hiyo wameuliwa mwezi huu katika nchi jirani ya Angola kutokana na ukandamizaji mkubwa wa polisi ya Angola katika machimbo ya madini ya almasi ya Artisanal. Polisi ya Angola imekanusha vikali tuhuma hizo.
Angola ambayo ni nchi ya tano duniani kwa uzalishaji mkubwa wa madini ya almasi katika wiki za karibuni ilianzisha oparesheni za kuwasaka na kuwafukuza makumi ya maelfu ya watu waliokuwa wakijihusisha na uchimbaji wa almasi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ili kuvutia uwekezaji zaidi wa makampuni binafsi.
Walinzi wa maeneo ya mpaka wa Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameeleza kuwa wengi wa raia waliofukuzwa ni kutoka katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hadi sasa mamia ya maelfu ya watu wameonekana kuwasili katika mpaka wakielekea mkoani Kasai nchini Kongo.
Taarifa zinasema kuwa machafuko makali zaidi yametokea katika mji wa Lucapa umbali wa kilomita zisizopungua 100 kusini mwa mpaka na Kongo; yaani katika kitovu cha mkoa tajiri kwa madini ya almasi wa Lunda Norte. Watu walioshuhudia wameeleza kuwa polisi wa Angola waliuvamia mji huo na kuanza kuuwa makumi ya watu, kuchoma nyumba, kupora mali za watu na kuwalazimisha kuondoka. Hata hivyo taarifa zinasema kuwa baadhi ya raia hao wa Kongo walikuwa wakiishi Angola kinyume cha sheria.