Waarabu wataka utatuzi wa kudumu wa mgogoro wa Libya
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League amesisitizia haja ya kutafutwa utatuzi wa kimsingi na wa kudumu wa mgogoro wa Libya.
Mtandao wa habari wa al Watan umemnukuu Ahmed Aboul Geit akisema hayo mjini Cairo, Misri wakati alipoonana na Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya na kuongeza kuwa, kupatikana utatuzi wa kisiasa na kuhitimishwa kipindi cha mpito huko Libya kunategemea jinsi yatakavyodhibitiwa makundi yenye silaha.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu aidha ameelezea kuweko tayari jumuiya hiyo kusaidia utatuzi wa mgogoro wa Libya kwa njia za kisiasa na kwa mujibu wa muongozo uliotolewa na Umoja wa Mataifa.
Tangu mwaka 2011, Libya haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja, baada ya Marekani na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika kampeni ya kumg'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.
Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zilishambulia kikatili miundombinu ya Libya na baadaye kuitelekeza nchi hiyo zikiacha silaha zikiwa zimeenea mikononi mwa makundi mbalimbali ya wanamgambo ambayo kila moja linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo.