Idadi ya vifo katika miripuko wa Somalia yaongezeka
(last modified Mon, 15 Oct 2018 07:51:09 GMT )
Oct 15, 2018 07:51 UTC
  • Idadi ya vifo katika miripuko wa Somalia yaongezeka

Idadi ya wahanga wa mashambulio mawili ya kujiripua kwa mabomu iliyotokea kusini magharibi mwa Somalia imeongezeka. Taarifa zinasema kuwa watu 20 wamepoteza maisha na wengine 40 wamejeruhiwa katika miripuko hiyo miwili iliyopishana kwa dakika chache tu.

Miripuko hiyo imetokea katika mji wa Baidoa wa kusini magharibi mwa Somalia baada ya watu waliokuwa wamejifunga mabomu kujiripua katika maeneo mawili tofauti.

Abdifatah Hashi, mkuu wa hospitali ya Baidoa amesema kuwa, watu waliothibitishwa kuuawa hadi hivi sasa katika miripuko hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia jana Jumapili imeongezeka na kufikia 20 huku 40 wengine wakijeruhiwa. Kabla ya hapo ilikuwa imetangazwa kuwa watu 16 wameuawa kwenye miripuko hiyo ya Jumamosi usiku. 

Mbali na umaskini wa kuchupa mipaka, Somalia inasumbuliwa mno na ukosefu wa usalama

 

Afisa mmoja wa polisi ya Baidoa, Abdulahi Mohamed amesema kuwa, mashambulizi hayo ya kigaidi yamelenga eneo lenye raia wengi ndio maana wahanga wake wote ni watu wa kawaida.

Afisa mwingine wa polisi anayejulikana kwa jina la Mohamed Adam amewaambia waandishi wa habari kuwa, watu wengi waliokuwa na hofu wamemiminika kwenye hospitali ya Baidoa kutafuta jamaa zao.

Miripuko hiyo imetokea siku moja kabla ya kutimia mwaka mmoja tangu lori moja liliporipuka mjini Mogadishu na kuua watu 500 shambulizi la kigaidi ambalo linahesabiwa kuwa baya zaidi kuwahi kuukumba mji huo kutoka kwa genge la kigaidi la al Shabab. 

Somalia ni moja ya nchi masikini zaidi na yenye usalama mdogo zaidi duniani.