Mashine za kupigia kura za Kongo zilizoibua makelele zaanza kuwasili
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana alisema kuwa mashine za kupigia kura katika uchaguzi wa mwezi Disemba zinazofanana na meza zitamalizika kuwasili nchini humo mwezi huu licha ya wanadiplomasia na upande wa upinzani kuwa na shaka kuwa mashine hizo huenda zikapelekea kuibiwa kura.
Rais Joseph Kabila wa Kongo anataraji kuondoka madarakani baada ya kushika hatamu za uongozi kwa miaka 17 kutokana na kuakhirishwa kwa muda mrefu uchaguzi wa rais ambao mara hii umepangwa kufanyika Disemba 23. Uchaguzi huo ambao ulipasa kufanyika kabla ya kumalizika muhula wa urais wa Kabila mwaka 2016; umeakhirishwa kwa kipindi kirefu jambo linalotilia shaka iwapo utafanyika kweli au la.
Iwapo utafanyika basi uchaguzi huu utakuwa mchakato wa kwanza wa kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani huko Kongo tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka Ubelgiji mwaka 1960. Henri Mova Sakanyi Naibu Waziri Mkuu na ambaye pia ni Waziri wa Usalama wa Kongo amesema kuwa makontena 180 yenye mashine hizo za kupigia kura kutoka Korea Kusini sasa yapo njiani baharini na hadi sasa makontena 15 yameshafika na yaliyosalia yatawasili nchini mwishoni mwa mwezi huu.