Oct 28, 2018 03:02 UTC
  • Jeshi la Nigeria laua Waislamu 10 wakishiriki Arubaini ya Imam Hussein AS

Wanajeshi wa Nigeria wameushambulia msafara wa Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wakishiriki katika maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein AS, viungani mwa mji mkuu wa nchi Abuja, na kuua shahidi kumi miongoni mwa waumini hao.

Mashahidi hao wameuawa kwa kupigwa risasi na maafisa usalama wa serikali katika kijiji cha Zuba, eneo la Gwagwalada viungani mwa mji mkuu Abuja, ambapo katika hujuma hiyo ya kinyama ya jeshi la serikali hapo jana, makumi ya watu wengine pia walijeruhiwa. 

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, waliouawa katika hujuma hiyo ya kinyama ni wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria, ambao walikuwa wamekusanyika katika maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein AS katika eneo la Zuba jimboni Niger.

Hata hivyo jeshi la Nigeria linadai kuwa, Waislamu hao walikataa kufuata amri ya kurejea nyuma walipotakiwa kufanya hivyo katika kituo cha upekuzi cha Zuma, kaskazini mwa Abuja. Hii sio mara ya kwanza kwa jeshi la Nigeria kuwaua kikatili na kuwashambulia Waislamu wa Nigeria.

Mabomu ya kutoa machozi yakifunika mkusanyiko wa waombolezaji wa Arubaini ya Imam Hussein AS mjini Abuja

Mwaka jana pia, wanajeshi wa Nigeria mbali na kuwafyatulia risasi waumini waliokuwa wakishiriki maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) katika mji mkuu Abuja na kuua kadhaa, lakini pia waliwavurumishia mabomu ya gesi ya kutoa machozi.

Wimbi la ukandamizaji wa kuchupa mpaka dhidi ya Waislamu nchini Nigeria lilianza mwezi Disemba mwaka 2015, baada ya jeshi la nchi hiyo kuvamia Husseinia ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna na kuua mamia ya Waislamu, mbali na kumtia mbaroni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria, Shiekh Ibrahim Zakzaky, ambaye yuko kizuizini hadi sasa.

Tags