UN: Machafuko ya Sudan Kusini yanazuia ugawaji wa misaada ya chakula
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa, machafuko yanayoendelea nchini Sudan Kusini yanazuia operesheni za kugawa misaada ya chakula kwa watu wanaosumbuliwa na njaa kali katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Ripoti ya WFP imesema kuwa, hakuna athari na vielelezo vya aina yoyote kwamba pande hasimu nchini humo zilitia saini makubaliano ya amani mwezi uliopita.
WFP imesisitiza kuwa, eneo la kusini magharibi mwa mji wa Wau katika mkoa wa Bahr el Ghazal ndilo linalosumbuliwa zaidi uhaba wa chakula.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa, mwezi uliopita utapiamlo katika eneo la Baggari nchini Sudan Kusini ulipanda juu ya kufikia asilimia 25 kutoka asilimia 4 ya mwaka jana.

Katika mji wa Wau askari wa jeshi la serikali ya Juba na wapiganaji wa makundi ya waasi wanatuhumiwa kushambulia raia na makazi yao. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeripoti kuwa, makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao na kuelekea misituni au kwenye vituo vya Umoja wa Mataifa kutokana na machafuko hayo. Ripoti ya shirika hilo imesema majeshi ya serikali ya Sudan Kusini yamezidisha unyanyasaji dhidi ya raia.
Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini, Lul Ruai Koang amekanusha madai hayo.