Ongezeko la vitendo vya kigaidi nchini Libya lautia wasiwasi Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49161-ongezeko_la_vitendo_vya_kigaidi_nchini_libya_lautia_wasiwasi_umoja_wa_mataifa
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa kuongezeka vitendo vya kigaidi katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Tripoli, linatia wasiwasi mkubwa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 31, 2018 12:14 UTC
  • Ongezeko la vitendo vya kigaidi nchini Libya lautia wasiwasi Umoja wa Mataifa

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa kuongezeka vitendo vya kigaidi katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Tripoli, linatia wasiwasi mkubwa.

Ghassan Salamé amesema hayo katika mazungumzo yake na Nasser Bourita, waziri wa mambo ya nje wa Morocco na kuhimiza kutafutwa njia zinazofaaa za kukomesha mapigano ya miezi kadhaa sasa pamoja na kutatuliwa hitilafu za ndani ya Libya sambamba na kuanzishwa mchakato wa kisiasa nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umetoa tamko kuhusu shambulizi la siku ya Jumapili la wanamgambo wa Daesh katika mji wa al Fuqahaa wa katikati mwa Libya na kulaani shambulio hilo. Raia wanne waliuawa na wengine 9 kujeruhiwa katika shambulizi hilo la kigaidi lililofanywa na genge la wakufurashaji la Daesh au ISIS.

Magaidi wa Daesh (ISIS) wakichinja watu nchini Libya

 

Vitendo vya kigaidi nchini Libya vimeripotiwa kuongezeka katika hali ambayo tarehe 10 Disemba mwaka huu, nchi hiyo inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa rais na bunge. 

Baadhi ya madola ya kigeni yanapinga kufanyika uchaguzi huo unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na yametishia kwamba hali itazidi kuharibika nchini Libya iwapo uchaguzi huo utafanyika.