Gaidi mmoja Algeria aelezea namna Marekani inavyoshirikiana na magaidi wa ISIS
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49285-gaidi_mmoja_algeria_aelezea_namna_marekani_inavyoshirikiana_na_magaidi_wa_isis
Gaidi mmoja wa Algeria ambaye wakati fulani alijiunga na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Syria ameiambia Mahakama ya al Dar al Baydhaa ya Algeria kuwa, wakati alipoingia Syria alipokewa na afisa mmoja wa jeshi la Marekani na kumpa mafunzo ya kutumia silaha yeye na wenzake kadhaa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 05, 2018 03:14 UTC
  • Gaidi mmoja Algeria aelezea namna Marekani inavyoshirikiana na magaidi wa ISIS

Gaidi mmoja wa Algeria ambaye wakati fulani alijiunga na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Syria ameiambia Mahakama ya al Dar al Baydhaa ya Algeria kuwa, wakati alipoingia Syria alipokewa na afisa mmoja wa jeshi la Marekani na kumpa mafunzo ya kutumia silaha yeye na wenzake kadhaa.

Televisheni ya Ennahar ya Algeria imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, gaidi huyo amezungumzia namna walivyopitisha siku zao za awali za kujiunga na genge la kigaidi la Daesh akisema kuwa, waliingia Syria kupitia Uturuki yeye na wenzake 11 na kupelekwa moja kwa moja kwenye kambi moja na huko wakapewa mafunzo ya kutumia silaha na afisa mmoja wa kijeshi wa Marekani.

Abdelqader Masahil, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria

 

Itakumbukwa kuwa, mwezi Disemba 2017, Waziri wa Sheria wa Algeria alitangaza kuwa raia wa nchi hiyo wasiopungua 226 wameelekea katika nchi za Iraq na Syria kwa ajili ya kujiunga na kundi la kigaidi la Daesh. Tayeb Louh alisema kuwa idara ya mahakama ya Algeria imetoa kibali cha kimataifa cha kutiwa mbaroni raia hao. Hata hivyo baada ya kusambaratishwa genge la wakufurishaji la Daesh huko Syria na Iraq, raia wa kigeni waliojiunga na magaidi hao waliamua kuhamia nchi nyingine na wengine kurejea katika nchi walizotoka, likiwa ni tishio kubwa kwa nchi hizo.

Mwishoni mwa mwaka 2017, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria alitangaza kuwa kundi la kigaidi la Daesh limewataka mamluki wake wahamie Libya, katika eneo la ukanda wa pwani na katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara barani Afrika baada ya kupata pigo huko Syria na Iraq. Abdulqader Masahil alizitaka nchi za Afrika kushirikiana zaidi katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.