Rwanda yasisitiza kuimarisha uhusiano na Iran
Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Richard Sezibera amepongeza uhusiano mzuri wa pande mbili kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitizia umuhimu wa kupanuliwa uhusiano huo katika nyuga mbalimbali.
Dakta Sezibera aliyasema hayo Jumanne katika mji mkuu Kigali, katika mkutano wake na Sayyid Morteza Mortazavi, Balozi wa Iran anayewakilisha nchi kadhaa ikiwemo Rwanda, Uganda na Burundi na kuongeza kuwa, serikali ya Rwanda ina hamu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Iran katika nyuga mbalimbali hususan tiba na kilimo.
Sezibera ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameongeza kuwa, serikali ya Kigali iko tayari kupanua uhusiano wa pande mbili na Iran katika uga wa uchumi na biashara, huku akiyaalika katika masoko ya nchi hiyo mashirika ya teknolojia ya Iran, hususan yale yanayoshughulikia masuala ya tiba na bidhaa za wanyama.
Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Rwanda ameyakosoa baadhi ya madola ambayo yamekuwa yakichukua maamuzi ya upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuwa na misimamo ya kindumakuwili ikija katika masuala ya ugaidi na haki za binadamu.
Kwa upande wake, Balozi Morteza Mortazavi ameashiria kuhusu uwezo mkubwa wa mashirika ya Iran haswa ya nishati, akisisitiza kuwa yako tayari kutoa huduma mbalimbali nchini Rwanda kama vile katika ujenzi wa vituo vya kawi, barabara, majengo ya makazi na ya kibiashara na vilevile katika sekta na mawasiliano.
Amesema serikali ya Tehran iko tayari kuyaarifisha makampuni ya Iran katika soko la nchi hiyo ya Kiafrika.