Tanzania yazidi kubanwa, Denmark na Benki ya Dunia zaifutia ruzuku, mikopo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49531-tanzania_yazidi_kubanwa_denmark_na_benki_ya_dunia_zaifutia_ruzuku_mikopo
Serikali ya Denmark imefuta mpango wake wa kuipa Tanzania msaada wa dola milioni 10 za Marekani, kulalamikia kile ilichotaja kama rekodi mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo, na matamshi 'yasiyokubalika' dhidi ya mashoga.
(last modified 2025-11-03T11:52:57+00:00 )
Nov 15, 2018 15:26 UTC
  • Tanzania yazidi kubanwa, Denmark na Benki ya Dunia zaifutia ruzuku, mikopo

Serikali ya Denmark imefuta mpango wake wa kuipa Tanzania msaada wa dola milioni 10 za Marekani, kulalamikia kile ilichotaja kama rekodi mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo, na matamshi 'yasiyokubalika' dhidi ya mashoga.

Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark ameandika kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter kuwa: Nina wasiwasi mkubwa kutokana na matukio hasi yanayoshuhudiwa hivi sasa nchini Tanzania, yakiwemo matamshi dhidi ya mashoga kutoka kwa mmoja wa makamishna. Kwa msingi huo, Denmark imefuta msaada wa crown milioni 65 za nchi hiyo (Dola milioni 9.88 za Marekani) kwa Tanzania. Denmark mwaka jana pekee iliipa Tanzania ruzuku ya crown milioni 349.

Hii ni katika hali ambayo, hapo jana Benki ya Dunia ilitangaza kufuta mkopo wa Dola milioni 300 za Marekani kwa Tanzania, kutokana na kile ilichosema ni matukio nchini Tanzania ambako mashoga na watu wengine wanaofanya mapenzi ya jinsia moja wanadhalilishwa na kubaguliwa. 

Siku chache zilizopita, World Bank ilitangaza kusimamisha ziara zake katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutokana na sakata hilo la mashoga.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1947, Benki ya Dunia imetoa fedha kwa miradi ya maendeleo zaidi ya 12,000 nchini Tanzania kupitia mikopo na misaada ya aina mbalimbali.

Sakata la mashoga nchini lilipamba moto hivi karibuni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuamua kuchukua hatua dhidi ya watu wenye tabia ya ushoga, jambo ambalo limeibua hisia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukoselewa na jumuia ya kimataifa. 

Serikali ya Tanzania imesema hatua za kiongozi huyo wa mkoa ni maoni yake binafsi, na kwamba serikali itaendelea kuheshimu haki za binadamu wote kama iliyo katika katiba ya nchi yake.