MONUSCO kuchukua hatua kali baada ya walinda amani kuuawa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49574-monusco_kuchukua_hatua_kali_baada_ya_walinda_amani_kuuawa_drc
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ulinzi wa amani Jean Pierre Lacroix amesema Kikosi cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO kitachukua hatua kali kukabiliana na makundi yenye silaha baada ya kuuawa walinda amani saba nchini humo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 17, 2018 12:42 UTC
  • MONUSCO kuchukua hatua kali baada ya walinda amani kuuawa DRC

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ulinzi wa amani Jean Pierre Lacroix amesema Kikosi cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO kitachukua hatua kali kukabiliana na makundi yenye silaha baada ya kuuawa walinda amani saba nchini humo.

Akizungumza na wanahabari Lacroix amesisistiza kuwa, MONUSCO itachukua hatua kali ili kudhoofisha uwezo wa makundi hayo, hasa waasi wa ADF, kundi ambalo linadhuru watu pamoja na kuzuia juhudi za kupambana na Ebola. Lacroix amesema makundi yenye silaha yamekuwa yakiwafanyia watu ukatili mkubwa kwa miaka mingi huko Kivu Kasakazini.

Akithibitisha vifo vya askari hao Lacroix amesema, sita wanatoka Malawi na mmoja anatoka Tanzania pamoja na askari 15 wa vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Askari hao waliuawa Jumatano kwenye maeneo ya Beni huko Kivu Kaskazini wakati wa operesheni ya pamoja dhidi ya kundi la ADF ambalo lipo DRC na Uganda.

Askari wa MONUSCO nchini DRC

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wapiganaji hao wa Uganda walifanya tena mashambulio dhidi ya ngome za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuua watu 13 mbali na kuwateka nyara watoto wasiopungua 12.

Aidha tarehe 22 Septemba pia raia 14 na wanajeshi 4 wa serikali ya Kongo DR  waliuawa katika shambulio lililodaiwa kufanywa na waasi wa Uganda wa ADF, mwezi mmoja baada ya genge hilo kufanya mashambulio mengine katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC na kuua watu sita.

Waasi wa Uganda wa ADF walianzisha harakati zao mashariki mwa Kongo tangu mwaka 1994 na katika miaka hiyo yote wameuwa mamia ya raia wa eneo hilo.