Watu 7 wauawa katika shambulizi la ADF nchini DRC
Raia sita na mwanamgambo mmoja wameuawa katika shambulizi la wapiganaji wa ADF wa Uganda, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ofisa Mkuu wa mji wa Beni, Donat Kibwana amesema hujuma hiyo ilifanyika usiku wa kuamkia jana, katika mji wa Oicha, umbali wa kilomita 30 kaskazini mwa Beni, mashariki mwa nchi.
Msemaji wa jeshi la Kongo DR, Kapteni Mak Hazukay amethibitisha kutokea mashambulizi hayo yaliyotokea chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu nchini humo.
Mashambulizi hayo yalipelekea kufanyika maandamano ya wananchi katika mji wa Oicha, karibu na Beni wakilalamikia kudorora kwa hali ya usalama na kukithiri mashambulizi ya wanamgambo wa ADF.
Haya yanajiri siku chache baada ya askari 8 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO kuuawa na wanamgambo hao wa ADF, huko Beni katika eneo la Kivu Kaskazini, huku 10 wakijeruhiwa na mmoja akitoweka.
Hii ni katika hali ambayo nchi hiyo ya katikati ya Afrika inaendelea kushuhudia kampeni za uchaguzi wa rais ambao umepangwa kufanyika tarehe 23 ya mwezi ujao wa Disemba.