Juhudi za kupambana na ugaidi barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49845-juhudi_za_kupambana_na_ugaidi_barani_afrika
Kufuatia kushamiri na kuenea harakati za makundi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali duniani hasa Afrika, nchi washiriki wa mkutano wa pili wa kimataifa wa kupambana na ugaidi uliofanyika katika mji mkuu wa Algeria, Algiers zimesisitizia ulazima wa nchi za magharibi mwa Afrika kushirikiana pamoja katika kupambana na janga hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2018 07:51 UTC
  • Juhudi za kupambana na ugaidi barani Afrika

Kufuatia kushamiri na kuenea harakati za makundi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali duniani hasa Afrika, nchi washiriki wa mkutano wa pili wa kimataifa wa kupambana na ugaidi uliofanyika katika mji mkuu wa Algeria, Algiers zimesisitizia ulazima wa nchi za magharibi mwa Afrika kushirikiana pamoja katika kupambana na janga hilo.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 30 za Afrika, Asia, Ulaya na Amerika pamoja na wawakilishi wa asasi na jumuiya 40 za ndani ya Algeria, za kieneo na kimataifa, hadhirina walijadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya usalama ya eneo la Sahel na jangwa la Afrika, mchango wa jumuiya na taasisi mbalimbali katika kudhamini fedha kwa makundi ya kigaidi na matatizo na changamoto zinazozikabili nchi za magharibi mwa Afrika kutokana na kurejea magaidi katika nchi hizo. Aidha wametilia mkazo haja ya nchi zote kufanya juhudi na kushirikiana pamoja kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi.

Japokuwa nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto nyingi katika nyuga za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama, lakini kuwepo makundi ya kigaidi barani humo na hofu ya kuenea harakati za makundi hayo katika nchi tofauti za bara hilo, sasa limekuwa ndilo jakamoyo kuu ambalo haliwahamanishi viongozi wa Kiafrika pekee, lakini linazitia kiwewe nchi za Ulaya pia.

Kuongezeka matatizo ya ndani katika nchi nyingi za Afrika kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine mabadiliko yanayojiri kikanda na kimataifa, vimeufanya ugaidi kuwa changamoto muhimu zaidi inayolikabili bara la Afrika. Kwa upande wa ndani, hali duni ya uchumi inayoshuhudiwa katika nchi nyingi za bara hilo pamoja na ufukara na ukosefu wa ajira vimesababisha Waafrika wengi hususan wa tabaka la vijana wavutiwe kujiunga na makundi ya kigaidi kwa njia ya kurubuniwa na kushawishiwa kupata fedha na ajira. Lakini pia hali ya kisiasa inayotawala katika nchi za Afrika Kaskazini, kuendelea kukosekana uthabiti wa kisiasa nchini Libya ambayo ni moja ya nchi muhimu zaidi za eneo hilo, na vilevile hali tete ya kiusalama inayoshuhudiwa nchini Mali vimechangia kushamiri na kupanuka wigo wa harakati za makundi ya kigaidi barani humo.

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabab la Somalia

Kwa upande mwingine, katika uga wa kimataifa pia mabadiliko ya kieneo na kisiasa, kusambaratishwa makundi ya kigaidi katika nchi nyingi za Magharibi ya Asia ikiwemo Iraq na Syria, na vilevile uingiliaji wa madola ya Magharibi, vimezidisha hofu na wasiwasi wa kurejea magaidi katika maeneo mengi zaidi ya bara la Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Nasser Bourita anaizungumzia nukta hiyo kwa kusema: Kuna magaidi zaidi ya elfu kumi wa makundi mawili ya Daesh na Al-Qaeda barani Afrika, ambapo kundi la Daesh limeelekeza hujuma na mashambulio yake katika akthari ya maeneo ya bara hilo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Nasser Bourita

Japokuwa tangu kitambo kirefu nyuma na kwa kutumia visingizio tofauti nchi za Magharibi zimejipenyeza na kujikita katika nchi mbalimbali za Afrika, lakini hivi sasa hatari ya kuenea harakati za kigaidi barani Afrika na wimbi lake kusambaa hadi ndani ya ardhi za nchi za Ulaya, hususan baada ya mashambulio ya kigaidi yaliyotokea katika miaka ya karibuni kwenye nchi kadhaa za bara hilo, vimezifanya nchi hizo zilipe zingatio maalumu suala la kupambana na ugaidi na kuongezwa kiwango cha ushirikiano wa kimataifa. Katika uwanja huo, kwa muda sasa Ufaransa imekuwa ikizungumzia mpango wa kutoa msaada wa kijeshi kwa ajili ya kuunda kikosi cha askari wa eneo la Sahel kwa ajili ya kupambana na ugaidi katika eneo hilo, lakini hakuna hatua za maana za kivitendo zilizochukuliwa hadi sasa kuhusiana na suala hilo.

Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania

Katika hali kama hii, viongozi wa nchi za Afrika wameamua kutilia mkazo zaidi kuongeza kiwango cha ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kupambana na ugaidi, wakiwa na dhamira pia ya kubuni njia za kivitendo za kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiusalama kwa lengo la kuleta amani na uthabiti barani humo. Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania analizungumzia suala hilo kwa kusema: Viongozi wa Afrika inapasa wawe na uratibu na muelekeo wa pamoja na kushirikiana kwa ajili ya kuzitatua changamoto hizi, kwa sababu mafanikio katika suala hili yatapatikana kupitia ushirikiano wa nchi zote.../