Unicef: Watoto milioni 1.5 wa CAR wanahitaji msaada wa dharura
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef umesema thuluthi mbili ya watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wapo katika hatari ya kupoteza maisha iwapo hawatafikishiwa msaada wa dharura haraka iwezekenavyo.
Ripoti mpya ya Unicef iliyotolewa Ijumaa hii imesema kuwa, watoto milioni moja na laki tano wa nchi hiyo ya Afrika wanahitaji msaada wa dharura, hilo likiwa ni ongezeko la watoto laki tatu, ikilinganishwa na mwaka 2016.
Christine Muhigana, mjumbe mwandamizi wa Unicef katika Jamhuri ya Afrika ya Kati amewaambia waandishi wa habari Ijumaa hii mjini Geneva kuwa, mgogoro wa kibinadamu unaoshuhudiwa hivi sasa katika nchi hiyo huenda ukawa mbaya mno kushinda ule wa mwaka 2013.

Mapema mwezi uliomalizika wa Novemba, Mpango wa Chakula Duniani WFP ulisema watu milioni mbili wapo katika hatari ya kupoteza maisha iwapo hawatafikishiwa msaada wa dharura wa chakula huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.