Chama kikuu cha upinzani Afrika Kusini chapinga marekebisho ya katiba
Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini kimetangaza kuwa, yumkini kikaenda mahakamani kusimamisha pendekezo la kufanyika marekebisho ya ardhi baada ya Bunge kupasisha ripoti inayoidhinisha kufanyika marekebisho ya katiba yatakayoruhusu kutwaliwa ardhi zinazomilikiwa na wazungu waliowachache bila ya kulipwa fidia.
Chama cha Democratic Alliance (DA) na baadhi ya makundi ya kutetea haki za binadamu yamekosoa vikali mpango huo wa serikali ya Pretoria yakisisitiza kuwa, utahatarisha haki ya kumiliki na kuwatia woga wawekezaji wa kigeni.
Umiki wa ardhi na mashamba ni suala nyeti sana nchini Afrika Kusini ambako ubaguzi wa rangi ungali umekita mizizi baada ya miongoni miwili ya kuondolewa madarakani utawala wa ugauzi (apartheid) uliowapokonya wazalendo weusi mashamba yao na kuyagawa kwa wazungu waliowachache.
Kwa msingi huo mwezi uliopita timu ya Bunge la Afrika Kusini ilitoa pendekezo la kufanyika marekebisho ya katiba yatakayowezesha kutwaliwa ardhi kubwa na mashamba yanayomilikiwa na wazungu wachache bila ya kulipwa fidia.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini aliyechukua nafasi ya Jacob Zuma mwezi Februari mwaka huu, amelipa kipaumbele kikubwa suala la kugawa ardhi kwa wazalendo weusi katika jitihada zake za kukiunganisha tena chama tawala cha ANC na kupata uungaji mkono wa umma kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo mwakani.