Ripoti: Marekani ina vituo vya kijeshi vya siri katika nchi za Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49976-ripoti_marekani_ina_vituo_vya_kijeshi_vya_siri_katika_nchi_za_afrika
Tovuti ya habari ya Intercept imefichua habari za kuwepo kambi za kijeshi za siri za Marekani katika nchi kadhaa za Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2018 12:58 UTC
  • Ripoti: Marekani ina vituo vya kijeshi vya siri katika nchi za Afrika

Tovuti ya habari ya Intercept imefichua habari za kuwepo kambi za kijeshi za siri za Marekani katika nchi kadhaa za Afrika.

Tovuti hiyo imefichua nyaraka za siri kuhusu kambi hizo za kijeshi za Marekani barani Afrika kwa kutumia Sheria ya Uhuru wa Habari.

Nyaraka hizo zimemnukuu Peter E. Teil, Mshauri wa Masuala ya Sayansi wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani Afrika (Africom) akisema kuwa, kuna vituo 34 vya kijeshi ambavyo havijatangazwa hadharani au kuwekwa wazi na serikali ya Washington katika nchi za Somalia, Libya na Niger.

Tovuti ya habari ya Intercept imemnukuu Adam Moore, Naibu Mhadhiri wa somo la Jografia katika Chuo Kikuu cha California nchini Marekani akisema kuwa, ni muhali kwa Marekani kudai kuwa uwepo wake wa kijeshi barani Afrika ni mdogo, ilhali ina vituo vya siri na dhahiri katika nchi za Somalia, Djibouti, Kenya, Libya, na katika nchi za eneo la Sahel; Cameroon, Chad, Niger, Mali, na Burkina Faso.

Wanajeshi wa Marekani katika moja ya nchi ajinabi

More ameashiria pia hatua ya Washington ya kujenga kituo cha ndege zisizo na rubani (drone) za kijeshi nchini Niger kwa shabaha eti ya kukabiliana na makundi ya kigaidi.

Kituo hicho cha drone kinachojengwa katika mji wa Agadez nchini Niger ni moja vya vituo vikubwa zaidi kuwahi kujengwa na Marekani katika nchi ajinabi.

Marekani inaendelea kupanua satua yake na kujenga vituo vya kijeshi katika nchi za Afrika kwa visingizo mbalimbali.