Hatima isiyojulikana ya watoto 15,000 wahanga wa machafuko Sudan Kusini
(last modified Thu, 13 Dec 2018 15:31:57 GMT )
Dec 13, 2018 15:31 UTC
  • Hatima isiyojulikana ya watoto 15,000 wahanga wa machafuko Sudan Kusini

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, kutokana machafuko na mapigano ya miaka mitano huko Sudan Kusini, hatima ya watoto 15,000 haijulikana kutokana na kutoweka au kukutengana na wazazi wao.

Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) iliyotolewa leo imeeleza wasiwasi wake ikisema kuwa, baada ya kupita miaka mitano ya vita na machafuko katika nchi changa zaidi barani Afrika ya Sudan Kusini, kuwapata watoto na kuwaunganisha na wazazi au familia zao limekuwa tatizo kubwa na kwamba, jambo hilo huchukua miezi kadhaa na wakati mwingine miaka.

Shirika la UNICEF limetahadharisha kwamba, watoto ambao wamepoteana na kutengana na wazazi wao na kubakia peke yao wanakabiliwa na hatari zaidi ya kukumbwa na vitendo vya utumiaji mabavu, miamala mibaya na kutumiwa vibaya.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Kadhalika Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema kuwa, makubaliano ya amani yaliyotiwa saini hivi karibuni baina ya pande zinazozozana huko Sudan Kusini inaweza kuwa fursa muhimu ya kuongeza juhudi kwa ajili ya kuwafikisha watoto kwa ndugu na familia zao na misaada mingine ya kibinadamu.

Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.