Ethiopia yaondoa wanajeshi wake katika mpaka na Eritrea
Katika kile kinachoonekana ni ishara ya kuendelea kuimarika uhusiano wa Asmara na Addis Ababa, jana Ijumaa serikali ya Ethiopia ilitangaza habari ya kuviondoa vikosi vyake vya jeshi katika mpaka na Eritrea.
Meja Jenerali Asrat Denero, Kamanda Mkuu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Ethiopia eneo la Magharibi amesema uhusiano wa nchi mbili hizo jirani ni mzuri sana kwa sasa, na hivyo serikali ya Addis Ababa haioni haja ya kubakia wanajeshi wake katika mpaka wa nchi mbili hizo.
Denero amesema, "Hakuna tena tishio mpakani, wanajeshi wetu waliokuwa katika mpaka wa Eritrea tutawatuma sehemu nyingine."
Katikati ya mwezi Julai mwaka huu pia, serikali ya Eritrea iliwaondoa wanajeshi wake katika mpaka wake na Ethiopia uliokuwa ukilindwa vikali.

Kadhalika ndege ya kwanza ya wasafiri kutoka Ethiopia ilitua katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20, mwezi huohuo, baada ya pande mbili hizo kuhuisha uhusiano wao.
Julai 9, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki walisaini makubaliano ya kukomesha uhasama na kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia katika hafla iliyofanyika mjini Asmara. Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993 na kukata uhusiano wa pande mbili.