Amisom: Hatujahusika na kukamatwa kamanda wa zamani wa al-Shabaab
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, Amisom kimekanusha madai kuwa kilihusika katika operesheni ya kumtia mbaroni aliyekuwa Naibu Kamanda wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab na pia msemaji wa zamani wa genge hilo la ukufurishaji, Mukhtar Robow Abu Mansur.
Iliarifiwa kuwa, Robow ambaye mwaka jana alijisalimisha kwa jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, alikamatawa siku ya Alkhamisi na wanajeshi wa Ethiopia ambao wako chini ya Kikosi cha Amisom.
Ingawaje jeshi la Ethiopia halijatoa taarifa kuhusu kadhia hiyo, lakini taarifa hiyo ya Amisom imejitenga na madai ya kuhusika na kukamatwa kiongozi huyo wa nambari mbili wa zamani wa al-Shabaab.
Ofisa mmoja wa Idara ya Intelijensia ya Somalia ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema Robow ambaye hivi karibuni alitangaza akiwa mjini Baidoa kuwa atagombea urais wa jimbo hilo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba 19, alikamatwa na maafisa wa idara hyo na kusafirishwa hadi mji mkuu Mogadishu.
Wizara ya Usalama wa Ndani nchini humo ilisema kuwa, Robow amekamatwa kwa kufanya kampeni licha ya kuambiwa kuwa hawezi kuruhusiwa kugombea kiti hicho katika jimbo la Kusini Magharibi kwa kuwa angali chini ya vikwazo vya jamii ya kimataifa ikiwemo Polisi ya Kimataifa Interpol.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, watu 11 akiwemo askari mmoja wa Ethiopia wameuawa katika ghasia zilizozuka baada ya kukamatawa Robow, kati ya wanajeshi hao wa Amison na watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani wa al-Shabaab waliokuwa wamejizatiti kwa silaha.