Watu 45 wauawa katika mapigano ya kikabila Kongo DR
Watu 45 wameuawa katika ghasia za kikabila zilizotokea magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hayo yamesema na Gentiny Ngobila, Gavana wa mkoa wa Mai-Ndombe ambaye ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, watu wengine 60 wamejeruhiwa katika mapigano hayo ya kikabila yaliyotokea kati ya Disemba 15 na 16, nyakati za usiku.
Katika hatua nyingine, mtu mmoja aliuawa hapo jana katika ghasia zilizozuka katika mji wa Tshikapa, eneo la katikati la Kasai, huku wengine 80 wakijeruhiwa siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.
Watu sita wameuawa kufikia sasa katika machafuko ya kikabla ya uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu wa Ijumaa wiki hii, Disemba 23, 2018.
Hapo jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilizitaka pande zote za kisiasa nchini humo kujiepusha na ghasia na uchochezi, ikiwa zimesalia siku nne tu kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Kushtadi ghasia hizo kumezidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kukaririwa machafuko kama yale yaliyoshuhudiwa katika chaguzi za mwaka 2006 na 2011 nchini humo.