Wapinzani: Waliouawa katika 'maandamano ya mkate' Sudan ni 22
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50360-wapinzani_waliouawa_katika_'maandamano_ya_mkate'_sudan_ni_22
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Sudan, Sadiq al-Mahdi amedai kuwa watu waliouawa na maafisa usalama katika maandamano ya kulalamikia kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama mkate na hali mbaya ya uchumi ni 22.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2018 03:53 UTC
  • Wapinzani: Waliouawa katika 'maandamano ya mkate' Sudan ni 22

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Sudan, Sadiq al-Mahdi amedai kuwa watu waliouawa na maafisa usalama katika maandamano ya kulalamikia kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama mkate na hali mbaya ya uchumi ni 22.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Omdurman, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Nile, al-Mahdi amesema upinzani unapinga vikali utumiaji wa nguvu kupita kiasi wa maafisa usalama kukabili maandamano ya wananchi. Amesisitiza kuwa serikali inawahadaa walimwengu kwa kutangaza idadi ndogo ya watu waliouawa.

Hapo jana Idara ya Upelelezi ya Sudan ilisema mtu mmoja ameuawa na kufanya idadi ya watu waliopoteza maisha katika maandamano hayo ya siku kadhaa sasa kufikia watu tisa.

Kinara huyo wa upinzani nchini Sudan ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa kitaifa na kimataifa wa mauaji ya waandamanaji hao.

Wakati huohuo, wanachama 14 wa muungano wa upinzani wa National Consensus Forces wametiwa mbaroni wakituhumiwa kuchochea maandamano hayo.

Maandamano ya Mkate Sudan

Serikali ya Khartoum inasisitiza kuwa, mtandao wenye makao yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambao una uhusiano na Israel umeingiza mamia ya waasi nchini Sudan kwa shabaha ya kuchochea machafuko nchini humo.

Maandamano kama haya ya sasa ya kulalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu na hali mbaya ya uchumi yalizuka tena mwezi Januari mwaka huu, lakini vyombo vya usalama vikafanikiwa kuyadhibiti baada ya kuwakamata viongozi waandamizi wa upinzani.