Maporomoko ya udongo yaua watu 5 Bukavu, Kongo DR
Maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa yamesababisha watu watano kupoteza maisha katika mkoa wa Bukavu, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ofisa wa serikali katika mkoa huo, Hypocrate Marume ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "miili mitano ya wanawake wanne na mtoto mmoja imepatikana katika kijiji cha Kadutu, baada ya kutokea maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha usiku kucha katika mkoa wa Bukavu."
Meya wa mji huo, Munyole Kashama amethibitisha kutokea vifo hivyo na kuongeza kuwa, watu wengine wanne wamejeruhiwa na kwamba shughuli za kusaka miili zaidi ya wahanga wa janga hilo zinaendelea.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikikumbwa mara kwa mara na matukio ya aina hiyo pamoja na mafuriko.
Agosti mwaka jana, watu 200 walipoteza maisha katika janga la kimaumbile la maporomoko ya udongo katika mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.