Mratibu wa mashambulizi yaliyoua makumi ya watu Mogadishu auawa Somalia
Mratibu wa mashambulizi ya kigaidi yaliyoua makumi ya raia na kujeruhi wengine wasiopungua 40 mwaka 2017 mjini Mogadishu ameuawa leo nchini Somalia.
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya jeshi nchini Somalia, Abdulle Bule amesema kuwa, Abdikadir Abukar ambaye ni mwanachama wa kundi la kigaidi la al Shabab alipatikana na hatia ya kupanga shambulizi la bomu dhidi ya hoteni moja mjini Mogadishu ambalo liliua watu kumi na kujeruhi wengine kadhaa. Abdikadir Abukar pia alipanga mashambulizi yaliyotokea karibu na Wizara ya Michezo na dhidi ya hoteli ya Kitaliano mjini Mogadishu yaliyoa watu 16.
Wapiganaji wa kundi la al Shabab waliotimuliwa mjini Mogadishu wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kuvizia dhidi ya maeneo ya umma na vituo vya askari wa kulinda amani wa kimataifa.
Jumamosi iliyopita pia watu 16 waliuawa katika hujuma ya kigaidi iliyofanywa na wanamgambo wa kundi hilo la al Shabab katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Waandishi habari watatu wa televisheni ya Kisomali ya Universal TV yenye makao yake London na miongoni mwa waliopoteza maisha katika shambulizi hilo la kigaidi.