Amnesty: Watu 37 wameuawa katika 'maandamano ya mkate' Sudan
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema makumi ya watu wameuawa katika makabiliano baina ya polisi na waandamanaji nchini Sudan.
Katika taarifa, shirika hilo lenye makao yake mjini London limesema lina taarifa za uhakika kuwa watu 37 wameuawa kufikia sasa katika maandamano ya wananchi ambao wanalalamikia ughali wa maisha nchini Sudan.
Licha ya Rais Omar al-Bashir wa Sudan juzi Jumatatu kuahidi kuchukua hatua za mageuzi ya kiuchumi ambazo zitaboresha maisha ya raia wa nchi hiyo, lakini wananchi wa Sudan jana Jumanne walimiminika tena mabarabarani kushiriki maandamano hayo.
Hiyo jana polisi ya Sudan ilitumia mabomu ya kutoa machozi sanjari na kufyatua risasi angani kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakielekea Ikulu ya Rais mjini Khartoum, kumshinikiza Rais Bashir ajiuzulu.
Vyama vikuu vya upinzani nchini Sudan vimeafikiana kuunga mkono maandamano hayo yanayofanywa na wananchi wa Sudan tangu Jumatano ya wiki iliyopita, kupinga sera za kiuchumi za serikali ya Rais Omar al-Bashir.
Katika hali ambayo vyombo vya usalama nchini humo vinashikilia kuwa waliouawa kufikia sasa ni watu tisa tu, lakini kiongozi mmoja wa upinzani hivi karibuni alisema waandamanaji 22 wameshauawa hadi sasa katika "Maandamano ya Mkate" nchini Sudan.