Msudan mwingine auawa katika maandamano
Baada ya kuuawa Msudan mwingine katika maandamano ya kupinga serikali, idadi ya wahanga waliopoteza maisha yao katika maandamano yaliyoanza wiki iliyopita, wameshafikia 38.
Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, maandamano yaliyoitishwa na vyama mbalimbali mjini Khartoum hiyo jana yamepelekea raia mmoja kuuawa baada ya kupigwa risasi kichwani na askari wa serikali.
Kabla ya kufanyika maandamano hayo ya jana Jumanne huko Khartoum, Shirika la Amnesty International la haki za binadamu lilitangaza kuwa, takwimu zilizokusanywa na duru za kuaminika zinaonesha kuwa kufikia jana polisi wa Sudan walishaua waandamanji 37 katika maandamano hayo yaliyoanza Jumatano iliiyopita.
Kwa muda wa wiki nzima sasa miji mbalimbali ya Sudan imashuhdua maandamano yanayolalamikia hali ngumu ya maisha na kupanda kwa bei za bidhaa.
Waandamanaji hao wanataka serikali ya Rais Omar al Bashir iondoke madarakani kwa kushindwa kuendesha vizuri nchi.
Serikali ya Sudan imetangaza hali ya hatari na marufuku ya kutoka nje katika baadhi ya mikoa ukiwemo wa Khartoum na imefunga shule na vyuo vikuu katika majimbo hayo.