'Maandamano ya Mkate' yazidi kuigubika Sudan, Rais al-Bashir akalia kuti kavu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50458-'maandamano_ya_mkate'_yazidi_kuigubika_sudan_rais_al_bashir_akalia_kuti_kavu
Maandamano ya mkate ambayo yamekuwa yakishushuhudiwa nchini Sudan kwa wiki moja sasa na ambayo yamechukua mkondo wa kisiasa, yamezidi kuigubika nchi hiyo na kuifanya serikali ya Rais Omar Hassan al-Bashir ikabiliwe na mashinikizo zaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 27, 2018 11:28 UTC
  • 'Maandamano ya Mkate' yazidi kuigubika Sudan, Rais al-Bashir akalia kuti kavu

Maandamano ya mkate ambayo yamekuwa yakishushuhudiwa nchini Sudan kwa wiki moja sasa na ambayo yamechukua mkondo wa kisiasa, yamezidi kuigubika nchi hiyo na kuifanya serikali ya Rais Omar Hassan al-Bashir ikabiliwe na mashinikizo zaidi.

Wanachuo wanaosomea taaluma ya udaktari katika chuo kikuu cha Gadarif, Mashariki mwa Sudan, leo waliungana na madaktari na waandishi wa habari wanaogoma, kushinikiza kujiuzulu Rais Omar Al Bashir.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walipiga nara za kuuilaani serikali na kumtaka Rais al-Bashir ang'atuke madarakani.

Madaktari wanaogoma wamewataka wafanyakazi wa taaluma nyingine, kujitokeza na kuwaunga mkono katika mgomo huu. Raia wa kawaida nao wanaendelea kujitokeza katika barabara za miji mbalimbali  ya Sudan na kumtaka Rais Bashir aondoke madarakani lakini pia wanalalamikia kupanda kwa bei ya mkate na mafuta.

Wakati huo huo, Rais wa Sudan amesisitiza waziwazi kwamba, hatasalimu amri mbele ya matakwa ya taifa la Sudan au matakwa ya wasaliti. Vilevile amewatahadharisha Wasudani kuhusu kile alichokiita uvumi na kusema kuwa, mwenendo wa marekebisho umeshika njia yake nchini Sudan.

Maandamano ya Wasudani yaliyoanza kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi yamepata sura nyingine na sasa waandamanaji wanataka kuondolewa madarakani serikali ya Omar al Bashir.

Watu wasiopungua 38 wameuawa hadi sasa katika maandamano hayo.

Serikali ya Sudan imetangaza hali ya hatari katika baadhi ya miji huku shule na Vyuo Vikuu vikifungwa uukiwemo mji mkuu Khartoum.