Tume ya Uchaguzi: Mshindi wa urais Madagascar ni Andry Rajoelina
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Madagascar imetangaza kuwa rais wa zamani wa nchi hiyo Andry Rajoelina ndiye aliyepata kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa urais wa Desemba 19, na hivyo ndiye rais wa baadaye wa kisiwa hicho kikubwa zaidi barani Afrika.
Kwa mujibu wa tume hiyo, Andry Rajoelina, ameshinda uchaguzi kwa kupata asilimia 55.66 ya kura na kumpiku mpinzani wake mkuu Marc Ravalomanana aliyepata asilimia 44.34 kura.
Marck Ravalomanana naye ni rais wa zamani wa Madagascar. Andry Rajoelina, mwenye umri wa miaka 44, ni maarufu sana kati ya wawanchi wa Madagascar kwani aliwahi kuwa meya wa mji mkuu Antananarivo mwaka 2007 na aliongoza nchi kwa miaka 5, kuanzia 2009 hadi 2013.
Kabla ya kutangazwa matokeo hayo, marais hao wa zamani wa Madagascar walijitangaza washindi wa uchaguzi huo. Ravalomanana ambaye anajulikana kwa jina la utani kama Papa aliwaambia wafuasi wake kuwa, "Tumeona matokeo, sio rasmi lakini ni sehemu ya matokeo hayo na yanaonesha kuwa Papa ameshinda."
Kwa upande wake Rajoelina alisema, "Mpinzani wangu amesema kuwa ameshinda, lakini ukweli wa mambo ni kuwa nambari 13 (yaani yeye Rajoelina) ameshinda Madagascar nzima."