Polisi Sudan wawashambulia waandamanaji wakitoka msikitini
Maafisa usalama nchini Sudan wamewashambulia kwa mabomu ya kutoa machozi, waumini wa Kiislamu waliokuwa wakishiriki 'maandamano ya amani' baada ya Sala ya Ijumaa, katika mji wa Omdurman, nje kidogo ya mji mkuu Khartoum.
Licha ya waandamanaji hao kusikika wakipiga nara za 'Amani...Amani!' lakini askari polisi wa nchi hiyo wamewavurumishia mabomu ya kutoa machozi, ambapo kadhaa miongoni mwao wamejeruhiwa.
Maandamano kama haya yameshuhudiwa hii leo baada ya Sala ya Ijumaa kaskazini mwa Khartoum, na pia katika mji wa Atbara wa mashariki mwa nchi, ambacho ni kitovu cha maandamano haya ya kulalamikia ugumu wa maisha.
Wakati huohuo, vyombo vya usalama vimewatia nguvuni shakhsia tisa wa upinzani, akiwemo Siddiq Youssef, kinara wa Chama cha Kikomunisti cha Sudan na viongozi wa vyama vya upinzani vya Ba'ath na Nasserist.
Huku maandamano hayo yakiendelea kushika kasi katika sehemu mbalimbali za nchi, madaktari na waandishi wa habari wameamua kugoma na kuingia mabarabarani kushiriki maandamano hayo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono matakwa ya haki ya wananchi wanaopigania uhuru na demokrasia nchini humo.
Makumi ya miji ya Sudan ukiwemo Khartoum, mji mkuu wa nchi hiyo inashuhudia maandamano makubwa ya wananchi tangu Jumatano ya wiki iliyopita ya tarehe 19 Disemba kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta.
Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty Internatioanal, hadi hivi sasa watu wasiopungua 38 wameshauliwa na maafisa usalama wa serikali ya Rais Omar al Bashir, ingawaje serikali yenyewe inashikilia kuwa watu waliouawa ni 19.