Watu 37 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Mali
Kwa akali raia 37 wa kabila la Fulani wameuawa katika mapigano ya kikabila katika eneo la Mopti nchini Mali.
Meya wa mji wa Bankass, Moulage Guindo amesema mauaji hayo yalitokea jana Jumanne katika kijiji cha Koulogon, katika eneo la Mopti katikati ya Mali.
Amesema waliofanya mashambulizi hayo walikuwa wamevalia kama wawindaji wa kabila la Donzo, na kwamba baadhi ya wahanga wa mauaji hayo ni watoto wadogo.
Mauaji hayo ya kikabila yametokea katika eneo la jangwani lenye usalama mdogo, na ambalo makundi yenye silaha huwa yanafanya mashambulizi ya mara kwa mara ndani ya ardhi ya Mali na katika nchi jirani za Magharibi na Katikati mwa Afrika.

Mapigano ya kikabila nchini Mali haswa baina ya kabila la kuhamahama la Tuareg na lile la wafugaji la Fulani hadi hivi sasa yameshaua mamia ya watu na kupelekea makumi ya maelfu ya wengine kukimbia makazi yao.
Katikati ya mwezi uliopita wa Disemba, watu wenye silaha ambao walikuwa wamepanda pikipiki waliua zaidi ya watu 40 wa kabila la Tuareg huko kaskazini mwa Mali, sehemu ambayo mapigano ya kugombania ardhi na maeneo yenye maji ni jambo la kawaida.