Maandamano yaendelea Sudan, wahadhiri wa vyuo vikuu watiwa nguvuni
Askari usalama wa Sudan wamewatia nguvuni wahadhiri wa vyuo vikuuu walioanzisha mgomo leo mjini Khaertoum na kukabiliana na waandamanaji kwa mabomu ya kutoa machozi.
Ripoti zinasema kuwa, askari usalama walishambulia mkusanyiko wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Khartoum walioanzisha mgomo na kutia mbaroni idadi kadhaa miongoni mwao.
Askari hao pia walitumia zana za aina mbalimbali yakiwemo mabomu ya kutoa machozi kwa ajili ya kutawanya maandamano ya wananchi waliokuwa katika barabara inayoelekea ikulu ya Rais Omar al Bashir. Barabara hiyo ni miongoni mwa maeneo manne yaliyotangazwa jana kwa ajili ya maandamano ya kuelekea Ikulu na kuwasilisha takwa la kuondoka madarakani Rais Omar al Bashir.
Ripoti zinasema kiongozi wa kundi la masufi wa Qadiriyya Azraq Taiba ametangaza uungaji mkono wake kwa waandamanaji hao na inasemekana kuwa migomo ya wafanyakazi wa umma inaanza kuenea katika miji mingine ya Sudan dhidi ya serikali ya al Bashir.
Jana pia askari polisi wa Sudan wametumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wapinzani wa serikali waliokuwa wakiandamana katika mji wa Omdurman, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Makumi ya waandamanaji wameuawa na mamia ya wengine kutiwa nguvuni tangu wananchi wa maeneo mbalimbali ya Sudan walipoanza maandamano ya kupinga sera za kiuchumi za serikali ya nchi hiyo tarehe 19 mwezi uliopita wa Disemba.