Jumuiya ya Madaktari nchini Sudan yaitisha mgomo wa nchi nzima
Jumuiya ya Madaktari nchini Sudan imeitisha mgomo wa nchi nzima ikilalamikia kuuawa kiholela waandamanaji kadhaa katika mji wa Omdurman.
Taarifa ya Jumuiya hiyo imevituhumu vyombo vya usalama vya Sudan kwamba, vilivamia hospitali kadhaa za nchi hiyo na kurusha mbomu ya kutoa machozi.
Kadhalika taarifa hiyo imebainisha kwamba, hospitali ya mji wa Omdurman ilishuhudia ufyatuaji risasi mkali ambao ulifika mpaka katika vyumba vya wagonjwa mahututi.
Tangu tarehe 19 Disemba 2018 hadi hivi sasa Sudan imekumbwa na maandamano makubwa ya nchi nzima kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na inasemekeana kuwa mgogoro kama huo haujawahi kuikumba Sudan katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema katikka ripoti yake kwamba, hadi sasa waandamanaji wasiopungua 40 wameuawa katika machafuko ya Sudan na limeilaumu serikali ya al Bashir kwamba inatumia risasi za moto kukabiliana na raia.
Hata hivyo serikali ya Sudan inapinga takwimu za idadi hiyo ya watu waliouawa na badala yake inasema kuwa, watu 19 ndio waliouawa tangu kuanza maandamano hayo ya mkate Disemba mwaka jana
Wafanya maandamano nchini Sudan wanalalamikia kupanda kwa bei ya mkate na bidhaa nyingine muhimu na wanakosoa siasa za kiuchumi za serikali ya Omar al Bashir.
Hivi sasa maandamano hayo yamechukua mkondo wa kisiasa, ambapo waandamanaji wanataka kuondoka madarakani Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo.