Kesi 40 zaripotiwa za waenezaji itikadi za mauaji ya kimbari Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5089-kesi_40_zaripotiwa_za_waenezaji_itikadi_za_mauaji_ya_kimbari_rwanda
Polisi wa Rwanda wameripoti kuwepo kesi 40 za hivi karibuni za wanaohusika na kueneza itikadi ya mauaji ya halaiki wakati wa wiki ya kuadhimisha mauaji ya halaiki iliyomalizika Jumatano iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2016 03:42 UTC
  • Kesi 40 zaripotiwa za waenezaji itikadi za mauaji ya kimbari Rwanda

Polisi wa Rwanda wameripoti kuwepo kesi 40 za hivi karibuni za wanaohusika na kueneza itikadi ya mauaji ya halaiki wakati wa wiki ya kuadhimisha mauaji ya halaiki iliyomalizika Jumatano iliyopita.

Msemaji wa polisi wa Rwanda Celestin Twahirwa, amesema wahusika wanafanyiwa uchunguzi kuhusu tuhuma za kueneza habari mbaya zinazolenga kukanusha na kupuuza mauaji ya halaiki katika jamii zao. Itikadi ya mauaji ya halaiki au kukana mauaji hayo ni kosa la jinai nchini Rwanda.

Twahirwa amesema kesi hizo zinajumuisha matamshi ya watu ambao wanaonekana kulenga kuumiza hisia za waathirika wa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994. Aidha amesema kuna wale ambao wamekana kufanyika mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi. Halikadhalika kumeripotiwa kesi ya mtu kusambaza sarafu ambazo hazitumiki tena ambazo zilitumika wakati wa utawala wa Grégoire Kayibanda. Kayibanda anatambulika kama mmoja kati ya wachochezi wakuu wa mauaji ya kimbari Rwanda. Halikadhalika polisi Rwanda wanasema wamemkamata mtu katika wilaya ya Nyarugenge ambaye alisema kukumbuka waliouawa kwa umati mwaka 1994 ni kupoteza wakati.

Watu wenye itikadi ya mauaji ya halaiki na wanaokana mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi hujitokeza zaidi Aprili kila mwaka wakati wa kukumbuka mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambapo Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani takribani milioni moja waliuawa katika kipindi cha siku 100. Hayo yanajiri wakati ambao hivi karibuni kulifichuka ripoti kuwa utawala haramu wa Israel ulihusika na mauaji hayo ya halaiki Rwanda kwa kupeleka idadi kubwa ya silaha nchini humo kinyume cha sharia za kimataifa.