Wasudan waendeleza maandamano ya mkate, wamtaka al Bashir ang'atuke
Maelfu ya Wasudan waliandamana tena jana Alkhamisi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuondoka madarakani serikali ya Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo.
Waandamanaji hao waliokuwa wakipiga nara zinazomtaka Rais Omar al Bashir aondoke madarakani walikabiliana na polisi na uskari usalama waliotumia mabomu na gesi ya kutoa machozi kwa ajili ya kutawanya maandamano hayo ambayo yameshuhudiwa katika miji kama Khartoum, el Obeid makao makuu ya Kordofan Kaskazini, Qadarif, Port Said na kadhalika.
Maandamano ya jana Alkhamisi yaliitishwa na Muungano wa Wasomi wa Sudan unaojumuisha jumuiya za madaktari, wahadhiri wa vyuo vikuu na wahandisi pamoja na vyama vya upinzani wakimtaka Rais Omar al Bashir aondoke madarakani.
Wananchi wa Sudan wamekuwa wakifanya maandamano katika majimbo karibu yote ya nchi hiyo wakilalamikia hali mbaya ya uchumi na ughali wa bidhaa.
Maandamano hayo yaliyopewa jina la "Maandamano ya Mkate" sasa yamechukua mkondo mpya na waandamanaji wanataka kuondolewa madarakani serikali ya Rais Omar al Bashir.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeripoti kuwa, watu wasiopungua 40 wameuliwa hadi sasa katika machafuko hayo, huku serikali ikishikilia kuwa ni watu 24 pekee.