Waandamanaji waendelea kuuawa Sudan, serikali yavituhumu vyama vya mrengo wa kushoto
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51038-waandamanaji_waendelea_kuuawa_sudan_serikali_yavituhumu_vyama_vya_mrengo_wa_kushoto
Idadi ya watu waliouawa kwa kupigwa risasi nchini Sudan katika "Maandamano ya Mkate" inaendelea kuongezeka baada ya kufariki dunia mwanafunzi wa chuo kikuu aliyepigwa risasi kichwani.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 21, 2019 23:52 UTC
  • Waandamanaji waendelea kuuawa Sudan, serikali yavituhumu vyama vya mrengo wa kushoto

Idadi ya watu waliouawa kwa kupigwa risasi nchini Sudan katika "Maandamano ya Mkate" inaendelea kuongezeka baada ya kufariki dunia mwanafunzi wa chuo kikuu aliyepigwa risasi kichwani.

Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Wasomi wa Sudan ambayo ndiyo inayosimamia maandamano ya sasa dhidi ya serikali ya Rais Omar al Bashir imesema kuwa mwanachuo al Fatih Omar Numeir aliyekuwa mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Khartoum aliaga dunia jana kutokana na jeraha la kupigwa risasi kichwani katika maandamano ya amani dhidi ya serikali ya al Bashir.  

Baada ya kutangazwa habari ya kifo cha mwanachuo huyo, mamia ya watu walifanya maandamano jana mjini Omdurman wakitaka kuondolewa madarakani serikali ya Khartoum.

Takwimu za serikali ya Sudan zinasema watu 27 wameuawa katika maandamano yanayopinga serikali yaliyoanza tarehe 19 Disemba kupinga ughali wa maisha na hali mbaya ya uchumi ambayo sasa yanataka kuondolewa madarakani serikali ya nchi hiyo. Hata hivyo jumuiya za kutetea haki za binadamu zinasema kuwa, zaidi ya waandamanaji 40 wameuawa kwa kupigwa risasi na askari usalama.

Maamun Hassan Ibrahim

Wakati huo huo Waziri wa Habari wa Sudan amevituhumu vyama vya mrengo wa kushoto kikiwemo Chama cha Kikomunisti na Harakati ya Ukombozi wa Sudan inayoongozwa na Abdul Wahid Nur kuwa vinahusika na uharibifu unaofuatana na maandamano ya wananchi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Maamun Hassan Ibrahim amedai kuwa, ushahidi unaonesha kuwa baadhi ya vyama vya siasa vinahusika na uharibu unaofanyika katika maandamano hayo.