Kinara wa kambi ya upinzani Cameroon atiwa nguvuni
Vyombo vya usalama vya Cameroon vimemtia nguvuni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani baada ya maandamano ya mwishoni mwa wiki iliyopita yaliyotawanywa na askari usalama kwa kutumia risasi za moto.
Maurice Kamto ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Renaissance Movement (MRC) amekuwa akiwahamasisha wananchi kufanya maandamano dhidi ya Rais Paul Biya wa Cameroon tangu aliposhindwa uchaguzi wa rais mwishoni mwa mwaka uliopita ambao alidai kwamba ulitawaliwa na udanganyifu.
Agbor Bala ambaye ni wakili wa Maurice Kamto amesema mteja wake amekamatwa na vyombo vya dola kutokana na maandamano ya mwishoni mwa wiki iliyopita. Watu kadhaa walijeruhiwa kwa kupigwa risasi katika maandamano hayo.
Rais Paul Biya wa Cameroon aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka jana anahesabiwa kuwa kiongozi mkongwe zaidi katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika na hufanya kikao na baraza lake la mawaziri mara moja kila baada ya miaka kadhaa. Kiongozi huyo hupitisha wakati wake mwingi katika safari za mara kwa mara za kibinafsi barani Ulaya.