Bunge la Sudan lasimamisha mpango wa kurefusha uongozi wa Rais Bashir
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51607-bunge_la_sudan_lasimamisha_mpango_wa_kurefusha_uongozi_wa_rais_bashir
Kamati ya Bunge la Sudan iliyotwikwa jukumu la kuifanyia marekebisho katiba kwa lengo la kurefusha uongozi wa Rais Omar al-Bashir wa nchi hiyo imesimamisha mpango huo.
(last modified 2026-01-03T09:06:27+00:00 )
Feb 17, 2019 08:06 UTC
  • Bunge la Sudan lasimamisha mpango wa kurefusha uongozi wa Rais Bashir

Kamati ya Bunge la Sudan iliyotwikwa jukumu la kuifanyia marekebisho katiba kwa lengo la kurefusha uongozi wa Rais Omar al-Bashir wa nchi hiyo imesimamisha mpango huo.

Kamati hiyo imeakhirisha kwa muda usiojulikana mkutano wake uliotazamiwa kujadili marekebisho hayo ya katiba ili kuondoa kikomo cha kugombea urais.

Kabla ya maandamano ya sasa dhidi ya serikali, aghalabu ya wawakilishi wa bunge la nchi hiyo walionekana kuunga mkono pendekezo hilo la kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi, ili kuondoa ukomo wa muda wa urais na kumwezesha al-Bashiri kugombea kiti hicho baada ya kumalizika muda wake wa sasa mwaka 2020.

Hata hivyo pendekezo hilo hivi sasa linaonekana kufifia kutokana na kushadidi maandamano ya wananchi, wanaomtaka Rais Bashir ajiuzulu.

Maandamano dhidi ya serikali Sudan yamesababisha makumi kuuawa

Kamati hiyo ya bunge la Sudan imesema imelazimika kuakhirisha vikao vya kujadilia marekebisho hayo, kwa kile ilichokitaja kama 'majukumu maalumu ya dharura'.

Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ambayo ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, yalichochewa na ughali wa maisha, lakini sasa yamebadilika na kuwa ni wimbi la kumtaka Rais al-Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani.