Kuakhirishwa uchaguzi sambamba na kuongezeka mivutano nchini Nigeria
Katika hali ambayo uchaguzi mkuu wa rais wa Nigeria ulikuwa umepangwa kufanyika Jumamosi tarehe 16 Februari, tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imeuakhirisha ghafla na kutangaza kuwa sasa utafanyika Jumamosi ijayo ya tarehe 23.
Hatua hiyo si tu kwamba imetia wasiwasi na kuwakasirisha Wanigeria waliowengi bali imepelekea wagombea wa vyama vikuu pinzani kukosoa uamuzi wa tume hiyo na kunyoosheana vidole vya lawama kuhusu chanzo cha kuakhirishwa uchaguzi huo. Uchaguzi wa rais wa Nigeria umeakhirishwa katika hali ambayo Muhammadu Buhari wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC) na Atiku Abubakar wa People’s Democratic Party’s (PDP) ndio wagombea wakuu wanaowania kiti hicho. Uchaguzi huo umeakhirishwa katika hali ambayo kwa muda mrefu sasa uvumi umekuwa ukienezwa kuhusu uwezekano wa kufanyika udanganyifu katika uchaguzi na hasa ikitiliwa maanani kwamba hatua ya Rais Buhari kuamua kugombe tena kiti cha urais wa nchi hiyo imepelekea wengi kuikosoa Tume Huru ya Uchaguzi ya Nigerea INEC pamoja na wanachama wa chama tawala kuwa wamekuwa wakifanya njama za kuchakachua uchaguzi huo. Olusegun Obasanjo rais wa zamani wa Nigeria huku akimkosoa Buhari kwamba anatumia kila njia kuhakikisha kuwa anachukua tena kiti hicho, ameandika katika barua ya wazi kwamba ana wasiwasi na shaka kubwa iwapo tume ya hivi sasa ya INEC inaweza kuendesha uchaguzi kwa msingi wa uadilifu, uwazi na kutopendelea upande wowote.
Baada ya kuakhirishwa ghafla uchaguzi wa rais wasiwasi wa kufanyika udanganyifu katika uchaguzi ujao umeongezeka, hata kama tayari tume ya uchaguzi imetangaza kuwa ililazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na matatizo ya kilojistiki. Pamoja na hayo, vyama viwili vilivyotajwa vinaendelea kulaumiana kuhusu kuwa na ushawishi juu ya utendaji wa tume ya uchaguzi. Kwa kadiri kwamba chama tawala kimeitaka tume hiyo kutotoa fursa kwa chama cha PDP kuzua mgogoro nchini, huku mgombea wa PDP Atiku Abubakar akikituhumu chama tawala kuwa kinafanya njama za kuzuia kufanyika uchaguzi huo, baada ya kupoteza matumaini ya kushinda uchaguzi. Wakati huohuo na baada ya kutangazwa kuakhirishwa uchaguzi, Rais Muhammad Buhari amewataka Wanigeria wote waendelee kuwa watulivu na kutojihusisha na vitendo vyovyote vya ghasia vinavyoweza kuzuia ustawi wa demokrasia nchini humo.
Mivutano ya uchaguzi imeongezeka nchini Nigeria katika hali ambayo nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu wa usalama, ugaidi wa Boko Haram, ufisadi, uhaba wa chakula na hali mbaya ya uchumi. Buhari alikuwa ameahidi kurudisha usalama Nigeria na kuing'oa kabisa mizizi ya magaidi wa Boko Haram, jambo ambalo ameshindwa kulitekeleza huku kipindi chake cha kwanza cha urais kikielekea ukingoni. Tatizo hilo la ugaidi bado ni moja ya changamoto kubwa zinazoikabili serikali yake nchini Nigeria. Hata kama Wanaigeria wanatumai kwamba watashuhudia mabadiliko makubwa ya kiusalama, kisisa na kiuchumi nchini baada ya kufanyika uchaguzi mkuu mwishoni mwa wiki, lakini inaonekana kuwa katika mazingira ya hivi sasa nafsi ya kufanyika uchaguzi salama, wa haki na uwazi ni changamoto kubwa inayowakabili wananchi hao.