Burundi inakataa kuondoa askari wake Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51677-burundi_inakataa_kuondoa_askari_wake_somalia
Marais wa Burundi na Somalia wameitisha kikao cha dharura cha nchi zenye askari katika Kikosi cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM, kujadili agizo la kutaka askari 1,000 wa kulinda amani wa Burundi waondoke Somalia kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Februari.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Feb 20, 2019 08:10 UTC
  • Burundi inakataa kuondoa askari wake Somalia

Marais wa Burundi na Somalia wameitisha kikao cha dharura cha nchi zenye askari katika Kikosi cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM, kujadili agizo la kutaka askari 1,000 wa kulinda amani wa Burundi waondoke Somalia kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Februari.

Umoja wa Afrika umeanza kuwapunguza askari wake wa kulinda amani Somalia na mwaka jana ulitaka askari 1,000 wa Burundi waondoke nchini humo kabla ya kumalizika mwezi huu wa Februari.

Burundi imepinga vikali amri hiyo ya kupunguza askari wake Somalia kutokana na kuwa mishahara wanayopata ni chanzo muhimu cha fedha za kigeni katika nchi hiyo ambayo ilikatiwa misaada ya wafadhili baada ya mgogoro wa kisiasa wa mwaka 2015.

Jana Rais Mohamed Abdullahi “Farmajo” wa Somalia alimaliza safari ya siku mbili Bujumbura ambapo alikukutana na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi. Marais hao waliafiki kuitishwe kikao cha dharura cha viongozi wa nchi ambazo zinachangia askari AMISOM.

Askari wa Burundi katika kikosi cha AMISOM Somalia

Umoja wa Afrika una askari 21,500 wanaosaidia kurejesha amani nchini Somalia na kukabiliana na magaidi wa kundi la Al Shabab.

Burundi ni ya pili kwa idadi kubwa ya askari wa AMISOM ambapo ina wanajeshi 5,400. Burundi hupata karibu dola milioni 18 kila miezi mitatu kutokana na askari wake kuhudumu katika kikosi cha AMISOM na hivyo kupunguza askari wake kutatoa pigo kubwa la kiuchumi kwa nchi hiyo.