Magaidi 19 wa al-Shabaab waangamizwa nchini Somalia
Wanachama wasiopungua 16 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameuawa katika makabiliano baina ya kundi hilo na vikosi vya usalama katika eneo la Bar Sanguni na Jamame mkoani Lower Juba, kusini mwa Somalia.
Kwa mujibu wa afisa usalama katika mkoa wa Jubaland, Abdi Nur Ibrahim, jeshi la Somalia limeshirikiana na vikosi vya usalama vya mkoa huo pamoja na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom) katika operesheni hiyo dhidi ya wanamgambo hao.
Huku hayo yakiripotiwa, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) chini ya mwavuli wa Amisom limetangaza habari ya kuwaua wapiganaji watatu wa kundi la al-Shabaab.
Kadhalika limefanikiwa kumkamata mwanachama wa genge hilo la kitakfiri katika operesheni iliyotokea kwenye mkoa wa mpakani wa Bura Hache.
Kwa mujibu wa Msemaji wa KDF, Luteni Kanali Paul Njuguna, jeshi hilo la Kenya lilipata silaha zilizokuwa zikitumiwa na magaidi hao, zikiwemo bunduki 2 za AK-47 na SLR na risasi kadhaa katika operesheni hiyo ya jana adhuhuri.
Mapema leo watu wanane wameuawa nchini Somalia na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko wa bomu katika soko la kuuza na kununua mifugo kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.